Waziri Mchengerwa awaongoza Rais wa FIFA, nchi 58 kuitazama Royal Tour

 


Na John Mapepele, Arusha

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, usiku wa Agosti 10, 2022 amewaongoza viongozi wakuu wa nchi 58 wa mashirikisho ya Soka kuangalia Filamu ya Royal Tour jijini Arusha.

Mhe. Mchengerwa amewaongoza kutazama  filamu hiyo iliyochezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia  Suluhu Hassan ambayo imewavutia  wengi kuiangalia na kuomba kutembelea maeneo mbalimbali.

Tayari makundi matatu ya washiriki yamejitokeza kutembelea Hifadhi za Ngorongoro, Serengeti na Zanzibar kuanzia kesho Agosti 11, 2022.

Kundi hili la viongozi limewajumuisha takribani watu mia tano ambao ni washiriki wa mkutano mkuu wa Shirikisho la soka Barani Afrika (CAF) ambao wamemaliza mkutano wao wa siku mmoja uliofanyika katika kituo cha kimataifa cha  Mikutano cha Arusha.

Mhe.  Mchengerwa amewakaribisha washiriki wote kutembelea vivutio vya utalii ambavyo Tanzania imebarikiwa ambavyo havipatikani sehemu nyingi duniani.

Aidha, amewashukuru Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na uongozi wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) kwa ushauri wa kuitaka Tanzania kuandaa mashindano ya soka ya Afrika (AFCON) ya mwaka 2027 kwa kushirikiana  na Uganda.

Amesema Tanzania ipo tayari kushirikiana na Uganda kwa kuwa nchi zote mbili ni majirani na ndugu pia zimekuwa na mashirikiano ya karibu katika mambo mengi kwa muda mrefu. 



Ametumia nafasi hiyo kuwakaribisha FIFA wakati wowote wanapofikiria kufanya mikutano yao kuja kufanyia Tanzania kwa kuwa Tanzania ina kila hitaji muhimu ya mikutano.
Tukio hilo pia lilipambwa na msanii Ray Vanny ambaye aliwaburudisha  vilivyo  washiriki hali iliyomuinua Rais wa FIFA Gianni Infantino kuanza kucheza singeli.

Kikundi cha Wana star pia kiliwainua washiriki kwa shangwe kufuatia mtindo wao wa kucheza na nyoka  na mahadhi ya kiafrika zaidi.

Kwa nyakati tofauti Rais wa FIFA na CAF wameishukuru Serikali ya Tanzania kwa mapokezi na maandalizi mazuri ya mkutano huo na kuahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika mihezo.


Comments

Popular posts from this blog

RAIS SAMIA AWAPA SALAMU TEMBO WARRIORS, MHE. MCHENGERWA ATOA AHADI NONO WAKISHINDA

Mhe. Mchengerwa awakabidhi kombe la UEFA mashabiki wa Real Madrid

Waziri Mchengerwa azindua zoezi la kitaifa la kusaka na kuibua vipaji "mtaa Kwa mtaa."